Jumamosi 8 Novemba 2025 - 20:56
Kwa nini Twala na Zubayr hawakufichua mahali alipozikwa Bibi Fāṭimah (a.s.)?

Kwa mujibu wa vyanzo vya kihistoria na riwaya, kufichwa kwa kaburi la Bibi Fātimah Az-Zahrā (a.s.) lilikuwa ni kwa ombi lake binafsi, ili watawala wa wakati huo wasihusike katika mazishi yake. Hata hivyo, swali muhimu ni hili: kwa nini watu kama Twalḥa na Zubayr — ambao inasemekana walihudhuria mazishi hayo — hawakufichua siri hiyo?

Kwa mujibu wa ripoti ya Shirika la Habari la Hawza, katika tafiti ya kihistoria na kiitikadi kuhusu matukio ya kipindi cha mwanzo wa Uislamu, suala la jinsi Bibi Fāṭimah (a.s.) alivyozikwa na sababu za kaburi lake kubaki siri limekuwa likichunguzwa na kuulizwa mara nyingi. Moja ya maswali hayo ni kwa nini wale wanaodaiwa kuhudhuria mazishi yake hawakutangaza mahali alipozikwa.

Chini ya utafiti wa Kituo cha Kitaifa cha Majibu kwa Maswali ya Dini, kama ulivyoelezwa katika kitabu Mālik Fadak, jibu lililotolewa nalo ni kama ifuatavyo:

Swali:
Ikiwa kufichwa kwa kaburi la Bibi Fāṭimah (a.s.) lilikuwa jambo muhimu kiasi hicho, kwa nini Twalḥa na Zubayr — ambao walihudhuria mazishi yake na baadaye wakawa maadui wa Imamu ‘Alī (a.s.) — hawakufichua mahali alipozikwa?

Jibu:
Bibi Fāṭimah (a.s.) hakuwa radhi na serikali ya wakati huo wala vitendo vyao, na hakutaka wahusike katika mazishi au sala ya jeneza lake. Kwa mujibu wa riwaya na ushahidi wa kihistoria, aliusia wazi kuwa kaburi lake libaki siri. Hili halina shaka. Kama jambo hilo lisingekuwa muhimu, asingelitoa wasia huo.

Kuhusu Twalḥa na Zubayr: kwanza, hakuna ushahidi wa wazi unaoonesha kuwa Twalḥa alihudhuria mazishi hayo. Kuhusu Zubayr, vyanzo vingi vya kihistoria havimtaji wazi kama mshiriki katika mazishi, bali vingine vinaashiria tu uwepo wake katika swala ya jeneza. Hivyo basi, ushiriki wake katika mazishi yenyewe si jambo lililothibitishwa.

Pili, hata kama tungeamini kuwa Zubayr alihudhuria, hakuna sababu ya kumfanya baada ya miaka 25 kufichua mahali alipokuwa amezikwa Bibi Fāṭimah (a.s.), kwani hatua hiyo isingemnufaisha yeye wala wafuasi wake. Kinyume chake, ingekuwa ni tendo la uchokozi na la kuumiza ambalo halina faida yoyote, na lingeweza hata kumharibia heshima yake kijamii. Kufanya hivyo kungeashiria kuwa alimkosea heshima binti wa Mtume (s.a.w.w.) kwa ajili ya maslahi ya kisiasa, jambo ambalo lingeathiri vibaya hadhi yake ya kijamii.

Zaidi ya hayo, Zubayr alikuwa na uhusiano wa nasaba na familia ya Mtume (s.a.w.w.), na hili peke yake lilikuwa kizuizi kwake kufanya jambo kama hilo. Kwa mujibu wa desturi za Waarabu — hasa miongoni mwa masharifu na wakubwa — waliepuka matendo ya kinyama na ya fedheha, kama vile kuua wanawake na watoto vitani, kwani yalihesabiwa kuwa ni doa la kudumu kwao. Mtume (s.a.w.w.) mwenyewe alikataza kupigana au kuwaua wanawake na watoto katika vita.

Hivyo, kushughulika na kaburi la Bibi Fāṭimah (a.s.) kwa njia yoyote kungehesabiwa kuwa aibu na fedheha kubwa, na watu wangeona kwamba waliposhindwa kumshinda Imamu ‘Alī (a.s.) vitani, walijaribu kumkera kwa kuvunja heshima ya kaburi la binti ya Mtume (s.a.w.w.).

Zaidi ya hayo, hata kama wangetaka kufichua mahali alipokuwa amezikwa, hilo lisingekuwa rahisi. Wakati huo Imamu ‘Alī (a.s.) ndiye aliyekuwa khalifa na mtawala wa dola, hivyo asingewaruhusu kufanya jambo kama hilo, na watu pia wasingelipokea vyema.

Natija ni kama ifuatavyo: Ushiriki wa Zubayr katika mazishi ya Bibi Fāṭimah (a.s.) si jambo lililo thabiti kihistoria. Lakini hata kama tungeukubali, kufichua mahali alipokuwa amezikwa kusingemletea faida yoyote, bali kungemletea hasara na fedheha.

Rejea:

1- Ibn Bābūyah, al-Amālī, uk. 658; ‘Ilal al-Sharā’i‘, juz. 1, uk. 185
2- Ibn Shahrāshūb, Manāqib Āl Abī Ṭālib, juz. 3, uk. 363
3- Al-Majlisī, Biḥār al-Anwār, juz. 43, uk. 183
4- Al-Ṭabarsī, I‘lām al-Warā
5- Al-Barqī, al-Maḥāsin

Lebo

Maoni yako

You are replying to: .
captcha